Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, amezindua rasmi Mfumo wa iCBS (Integrated Core Banking System) wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku akiupongeza kwa dhati mchango mkubwa wa wataalam wa ndani katika kuubuni na kuuendesha mfumo huo.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Dkt. Mpango amesema uundwaji wa mfumo huo kwa kutumia rasilimali watu wa ndani si tu mafanikio ya kiteknolojia, bali ni ushahidi wa uhuru wa kidijitali uliopatikana nchini, tofauti na kipindi cha nyuma ambacho kilitawaliwa na utegemezi kwa watoa huduma wa kigeni.
“Kwa kutengeneza Mfumo huu, tumedhihirisha kuwa tunaweza kujitegemea. Zaidi ya hayo, tumeongeza uwezo wa kudhibiti taarifa na mifumo yetu ya kifedha, jambo ambalo ni muhimu sana katika enzi hizi za uhalifu mkubwa wa kimtandao, changamoto za siasa za kimataifa na ushindani mkali wa kiuchumi,” alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu na kuimarisha mazingira wezeshi kwa taasisi za fedha kutekeleza majukumu yao ya kisheria.
Katika hatua nyingine, alizitaka taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa mifumo ya malipo, hususan Benki Kuu, TCRA na e-GA, kuhakikisha usimamizi thabiti na ulinzi wa mifumo hiyo dhidi ya hatari za uhalifu wa kimtandao. Alisema ni muhimu kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kufanya miamala ili kupunguza utegemezi wa fedha taslimu.
Akizungumza awali, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika ambapo Benki Kuu yake imeunda Mfumo Jumuishi wa Kibenki kwa kutumia wataalamu wake wa ndani na bajeti ya fedha za ndani bila msaada wowote wa fedha wala wa kiufundi kutoka nje ya nchi.
"Hii ni historia ya kipekee, kwani kwa kawaida mifumo mikuu ya kibenki ya aina hii hutengenezwa na makampuni makubwa ya TEHAMA duniani, lakini Benki Kuu ya Tanzania imeweza kutimiza hilo kwa mafanikio makubwa", alisema.
Uundwaji wa Mfumo wa iCBS unaashiria mwanzo wa zama mpya katika uendeshaji wa shughuli za Benki Kuu, ambapo unaleta ufanisi mkubwa wa kiutendaji na kuimarisha uwezo wa kusimamia shughuli za kifedha kwa weledi na teknolojia ya kisasa.