Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 5.75 kwa robo ya nne ya mwaka 2025 kama ilivyokuwa kwa robo ya tatu ya mwaka 2025 iliyoishia mwezi Septemba 2025.
Akizungumza katika mkutano na viongozi wa benki, taasisi za fedha na waandishi wa habari, Gavana wa BoT ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema uamuzi huu unatokana na makadirio ya Benki Kuu yanayoonesha kuwa uchumi utaendelea kukua na mfumuko wa bei utabaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 .
‘Uamuzi wa kutokubadili Riba hii umetokana na tathmini iliyofanyika kuhusu mwelekeo wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi. Mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.4 mwezi Agosti, na unatarajiwa kubakia, ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5. Wakati huohuo, makadirio ya BoT yanaonesha kuwa uchumi utaendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha’’, Amesema.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa sera ya fedha katika robo ya tatu ya mwaka ulifanikiwa kuhakikisha uwepo wa ukwasi wa kutosha kwenye uchumi ambapo ilipelekea kupungua kwa riba ya mikopo ya siku 7 baina ya mabenki.
"Benki Kuu ilitumia nyenzo zake za sera ya fedha, hususan mikopo ya muda mfupi kwa mabenki (reverse repo operations) kuongeza ukwasi kwenye uchumi. Kufuatia hatua hii, hali ya ukwasi iliimarika na kupelekea kupungua kwa riba ya mikopo ya siku 7 baina ya mabenki". Ameeleza Gavana Tutuba.
Kuhusu mwenendo wa uchumi nchini, Gavana amesema uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2024. Mwenendo huu ulichangiwa zaidi na shughuli za uchimbaji madini, kilimo, huduma za fedha na bima, ujenzi, na shughuli za uzalishaji viwandani.
Kwa upande wa Zanzibar, ameeleza kuwa uchumi ulikua kwa asilimia 6.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, sawa na ukuaji uliorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024. Ukuaji huu ulichangiwa zaidi na shughuli za utalii, ujenzi na kilimo.
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki nchini (TBA), Bw. Theobald Sabi, amesema kuwa ukuaji wa pato la taifa, kuongezeka kwa ukwasi wa fedha za kigeni, kuimarika kwa thamani ya shilingi pamoja na ufanisi wa sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo utalii, madini na kilimo, ni viashiria vinavyothibitisha uimara na ustahimilivu wa uchumi wa Tanzania.
Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) ni kiwango kinachowekwa na BoT kama rejea katika utekelezaji wa shughuli zake mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukopesha benki za biashara. Kiwango hiki huathiri riba za mikopo baina ya benki za biashara, ambazo zinapaswa kuwa ndani ya wigo wa ±2.0% ya CBR iliyowekwa.