Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetunukiwa tuzo ya Mshindi wa Kwanza katika kundi la mashirika ya kibiashara na yasiyo ya kibiashara, ikiwa ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuendeleza viwango vya juu vya utawala bora, uwazi na uwajibikaji wa taasisi.
Tuzo hiyo imetolewa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kukabidhiwa kwa Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma iliyofanyika jijini Arusha tarehe 24 Agosti 2025.
Vigezo vilivyotumika katika utoaji wa tuzo hiyo vilijikita katika utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi kwa kiwango cha juu, upatikanaji wa maoni chanya ya ukaguzi, uwazi katika kuchapisha taarifa za kifedha, pamoja na tathmini nzuri ya utendaji wa Bodi ya Wakurugenzi.
Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja za menejimenti, wafanyakazi na viongozi wa Benki Kuu katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa manufaa ya Taifa.