BoT yang’ara anga za kimataifa kwa Huduma Jumuishi za Fedha

Benki Kuu ya Tanzania imetunukiwa Tuzo Kuu ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha (Nestor Espenilla Jr. Financial Inclusion Innovation Award) inayotolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI) yenye nchi wanachama 84. 

Tuzo hii mashuhuri inalenga kutambua nchi wanachama wa AFI ambao wameonyesha juhudi kubwa katika ubunifu na matumizi ya teknolojia, pamoja na kutambua uongozi imara katika kuchochea kasi ya upatikanaji na matumizi ya Huduma Jumuishi za Fedha.

Tuzo hiyo ilipokelewa na Naibu Gavana anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Huduma Jumuishi za Fedha unaoendelea mjini Swakopmund, nchini Namibia. Bi. Msemo anaongoza ujumbe wa Benki Kuu unaoshiriki katika mikutano hiyo kama wawakilishi wa vikundi kazi na kamati za AFI.

Baadhi ya mambo yaliyoiwezesha Benki Kuu kuibuka kidedea ni utekelezaji madhubuti wa Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo (TIPS); kuanzishwa kwa mazingira ya majaribio ya ubunifu (Bank of Tanzania Fintech Regulatory Sandbox Regulations, 2024); mfumo wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi (SEMA na BoT); pamoja na matumizi ya msimbo milia wa malipo (QR Code) ujulikanao kama TANQR.

Aidha, Meneja, Idara ya Huduma Jumuishi za Fedha, Bi. Nangi Massawe ametambuliwa kupitia Tuzo za Uongozi wa Kiufundi za AFI (AFI Technical Leadership Awards). Tuzo hizi hutolewa kwa wataalamu kutoka nchi wanachama wa AFI ambao wameonyesha mchango mkubwa wa kiufundi, ushiriki wa hali ya juu katika kubadilishana maarifa, na kutoa mafunzo kwa nchi wanachama wengine ili kukuza ujumuishaji wa kifedha kupitia sera, mikakati na ubunifu wa kitaifa.

Mafanikio haya ni kielelezo cha uongozi thabiti wa Benki Kuu chini ya Gavana Emmanuel Tutuba katika kusimamia juhudi za kuongeza na kuchochea matumizi ya huduma za fedha kwa kutumia teknolojia. Hatua hizi zinalenga kuongeza ufanisi, kupunguza gharama, na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa na kuboresha maisha yao.