Tanzania imeendelea kuonesha utendaji imara wa uchumi mkuu ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwa mujibu wa ripoti ya kikanda iliyojadiliwa katika Mkutano wa 61 wa Kamati ya Magavana wa Benki Kuu (CCBG) za SADC, uliofanyika Gaborone, Botswana tarehe 11 Septemba 2025.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, alihudhuria mkutano huo pamoja na magavana wenzake kutoka nchi wanachama wa SADC.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa uchumi wa SADC ulipungua kasi ya ukuaji hadi asilimia 3.0 mwaka 2024 kutoka asilimia 3.8 mwaka 2023, huku nchi wanachama zikionesha mwenendo tofauti wa ukuaji. Tanzania iliibuka kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri zaidi, ikisajili ukuaji wa asilimia 5.5, wa pili kwa kasi zaidi katika kanda, unaochochewa na shughuli thabiti za kiuchumi ndani ya nchi.
Kuhusu mfumuko wa bei, ingawa wastani wa kikanda ulipungua hadi asilimia 9.0 mwaka 2024 kutoka asilimia 9.5 mwaka 2023, nchi nyingi za SADC zilibaki juu ya lengo la ulinganifu wa makroekonomia la asilimia 3% – 7%. Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi saba—pamoja na Eswatini, Lesotho, Mauritius, Msumbiji, Namibia na Afrika Kusini—zilizofanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei ndani ya kiwango kinachokubalika.
Kwa upande wa biashara, ripoti ilibainisha kuwa nchi nyingi za SADC ziliendelea kuwa waagizaji wa bidhaa kutoka nje. Hata hivyo, Tanzania ilijipambanua kwa kurekodi ziada ya biashara yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2, ikionyesha ufanisi mkubwa wa mauzo ya nje na mchango chanya katika ushirikiano wa kibiashara wa kikanda.
Kielelezo cha Muunganiko wa Uchumi Mkuu wa SADC pia kilithibitisha nafasi ya Tanzania kama moja ya nchi zinazofanya vizuri katika kudumisha utulivu wa uchumi mwaka hadi mwaka.
Mkutano wa 61 wa Kamati ya Magavana wa Benki Kuu (CCBG) za SADC ulioongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Afrika Kusini, Bw. Lesetja Kganyago, uliwapa fursa viongozi hao kujadiliana masuala mbalimbali ya kimkakati yanayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha usimamizi wa mabenki na utulivu wa sekta ya fedha, pamoja na maendeleo katika mifumo ya malipo.