Benki Kuu ya Tanzania leo Novemba 13, 2023 imeishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake katika kuwezesha utekelezaji wa sera ya fedha. Hayo yamesemwa na Naibu Gavana Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, wakati wa ziara ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliofanyika katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam.
“Benki Kuu inashukuru kwa ushirikiano mkubwa inaoupata kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jukumu lake la kutekeleza sera ya fedha, hali inayochangia ukuaji endelevu wa uchumi nchini”, alisema
Aidha, aliihakikishia kamati hiyo kuwa Benki Kuu itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha kwamba sera ya Uchumi wa Buluu inakuwa yenye tija katika kukuza uchumi wa taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi, Mhe. Mwanaasha Khamis Juma (MB), ameipongeza BoT kwa utendaji kazi wake na ushirikiano unaotoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika ziara hiyo, kamati ilipata fursa ya kujifunza Jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ambalo ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.
Majukumu mengine ya BoT ni pamoja na kutoa sarafu ya nchi, kusimamia mabenki na taasisi za fedha, kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo nchini, kuhifadhi akiba ya nchi ikiwemo fedha za kigeni na dhahabu; kutoa ushauri juu ya masuala ya uchumi na fedha kwa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.