Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeagizwa kuweka mkakati wa kukunua dhahabu kutoka kwa wauzaji na wachimbaji wa dhahabu nchini kwa bei ya soko.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Sita ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko, ameipongeza Benki Kuu kwa kuanza zoezi la kununua dhahabu ambapo mpaka sasa imeweza kununua na kusafisha dhahabu yenye uzito wa kilo 418.
“Wekeni mkakati wa kununua kila aina ya dhahabu kwa bei ya soko na muwafikie wachimbaji wadogo popote walipo, wapeni elimu, watawaletea kila kilo wanayochimba na tani 6 mnayotaka mtapata,” alisema.
Dkt. Biteko aliongeza kuwa kutumia nguvu au sheria haitosaidia zoezi hilo la ununuaji wa dhahabu bali Benki Kuu inapaswa kuwa karibu na wachimbaji wote na kushirikiana na Wizara ya Madini kuwafikia kupitia vyama vyao.
Pia, alisema uwepo wa viwanda vizuri vyenye teknolojia ya kisasa katika uchakataji na usafishaji wa madini ya dhahabu ndani ya nchi kumepelekea kujenga imani kwa wanunuzi mbalimbali akiwemo BoT tofauti na awali, kabla ya kuwepo kwa viwanda vya uchakataji na usafishaji kufikia kiwango cha asilimia 99.9.
Awali, akizungumza katika banda la BoT kwenye Maonesho hayo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa Tanzania imeingia katika historia ya nchi ambazo zinahifadhi dhahabu kama akiba ya nchi kwa kununua dhahabu iliyochimbwa na kusafishwa nchini.
“Katika Maonesho haya tunaendelea kuhamasisha wananchi waje kupata elimu na kufahamu namna ambavyo wanaweza kuuza dhahabu yao kupitia Benki Kuu. Nasisi katika kununua tunatumia bei ya soko kwa siku hio, alisema.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Dkt. Anna Lyimo, alisema kuwa BoT inafahamu uwepo wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo na wa kati ikiwemo elimu, mitaji na teknolojia wanayotumia kuchimbia dhahabu.
“Benki Kuu imekaa na wadau mbalimbali kama Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kuwafikia wachimbaji wadogo ambapo kupitia Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Ajili ya Mauzo ya Bidhaa za Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme), BoT itashirikiana na STAMICO kutoa udhamini wa mikopo kwa vikundi vya wachimbaji wadogo,” alisema.
Dkt. Lyimo aliongeza kuwa katika Maonesho hayo ya Sita ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini, Benki Kuu inatoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria ya fedha za kigeni, 2022 (Foreign Exchange Act,2022, ambayo imeelekeza kuwa mapato yote yanayotokana na mauzo ya nje ya nchi yarudishwae nchini ndani ya siku 90.