Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amevitaka Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kufanya kazi kibiashara ili kuendelea kuvikuza vyama hivyo na kuleta tija kwa wanachama.
Gavana Tutuba ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utendaji wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa mwaka 2022 jijini Mwanza, ambapo amesema ukuaji wa uchumi unaendana na uwepo wa SACCOS imara zenye kufanya kazi kiushindani ili kupata masoko ya huduma na bidhaa mbalimbali wanazozalisha.
“SACCOS za sasa zinatakiwa kufanya kazi kisasa ili kujitofautisha na zile za kale ambazo mwisho wake zilifilisika, fanyeni kazi zenu kibiashara ili muendelee kuwepo na kukua kiuchumi”, alisema.
Aidha, amesema serikali kupitia wizara ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga zaidi ya shilingi bilioni 700 ili kuhamasisha watanzania kuuza bidhaa nje ya nchi ili kuchagiza uchumi, ambapo ametoa rai kwa vyama hivyo kutumia fursa hiyo kuwa kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa zao ziwe na sifa ya kuuza nje ya nchi.
Pia, amewaasa wanachama, viongozi na watendaji wa SACCOS Tanzania kulinda rasilimali zao, kuboresha huduma na kutumia teknolojia za kisasa ili kuhimili ushindani uliopo katika sekta ya fedha.
“Tunatamani kuona SACCOS zinaendelea kukua na kushindana na taasisi nyingine kubwa za kifedha katika utoaji wa huduma bora, na sio kwa kuwa na fedha au mali nyingi zisizowanufaisha wanachama wao,” alisema.
Gavana Tutuba amewahakikishia wanachama, viongozi na watendaji wa SACCOS Tanzania kwamba Benki Kuu kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kufanya shughuli zao wakati wote.
“Wito wangu kwenu ni kufuata matakwa ya sheria, kanuni, miongozo na sera za vyama vyenu ili kuhakikisha kuwa kuna mifumo thabiti ya udhibiti wa ndani, pamoja na usalama wa fedha na mali za wanachama na vyama vyenu,” alisema.
Kwa upande wake, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), Dkt. Benson Ndiege, amesema wameweka mikakati mbalimbali katika kukuza SACCOS nchini ambapo miongoni mwa mipango iliyopo ni matumizi ya TEHAMA katika shughuli zinazofanywa na vyama hivo.
Dkt. Ndiege aliongeza kuwa kukamilika kwa taarifa ya utendaji wa SACCOS kunatoa nafasi ya kuendelea kuimarisha sekta hiyo na kuiwezesha jamii na wadau kufahamu hali ya uendeshaji, ukuaji na manufaa yapatikanayo kutokana na uwepo wa SACCOS nchini.