Skip to content
Huduma Jumuishi za Fedha zaing’arisha BoT kimataifa

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imetambuliwa miongoni mwa taasisi tatu bora kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion – AFI) duniani, kutokana na uongozi madhubuti katika sera za huduma jumuishi za fedha na juhudi za kupunguza pengo la kijinsia katika upatikanaji wa huduma za fedha.

Utambuzi huo ulitolewa kupitia vipengele mbalimbali vya tuzo na vyeti vya AFI, ikiwemo Tuzo ya Azimio la Maya (Maya Declaration Award), inayotambua mafanikio ya nchi katika kuweka, kupima na kutekeleza ahadi za kuendeleza huduma jumuishi za fedha.

Benki Kuu pia ilitambuliwa kwa nafasi yake katika utekelezaji wa Mpango Kazi wa Denarau (Denarau Action Plan), ambao unaweka msisitizo katika kuendeleza huduma jumuishi za fedha kwa wanawake na kuchukua hatua madhubuti za kupunguza pengo la kijinsia katika huduma za fedha. Aidha, Benki ilitambuliwa kwa juhudi za kuandaa na kutekeleza sera mbalimbali zinazochangia kupunguza pengo hilo.

Vyeti hivyo vya kutambuliwa vilipokelewa na Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa Jukwaa la Kimataifa la Sera za Huduma Jumuishi za Fedha la mwaka 2026, lililofanyika Port Moresby, Papua New Guinea, kuanzia tarehe 1 hadi 4 Septemba 2026.

Akizungumza katika mjadala uliobeba mada kuhusu “Afya ya Kifedha: Msingi wa Uchumi Himilivu na Mustakabali Jumuishi.”, Gavana Tutuba alieleza uzoefu na maendeleo ya Tanzania katika kuimarisha afya ya kifedha kupitia mfumo unganishi wa malipo ya kidijitali, sera na mikakati ya maendeleo ya sekta ya fedha, pamoja na programu za elimu na uwezo wa kifedha.

Aidha, alisisitiza kuwa upatikanaji wa huduma za fedha ni hatua ya mwanzo, na kwamba matokeo halisi yanapaswa kuonekana katika uwezo wa wananchi kusimamia mapato na matumizi yao, kuweka akiba, kutumia mikopo kwa tija, kukabiliana na misukosuko ya kifedha na kuboresha maisha yao.

Pia, Gavana Tutuba alipewa heshima ya kukabidhi Tuzo ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha ya Nestor Espenilla Jr. ya mwaka 2026 kwa Benki Kuu ya Zambia, iliyotwaa tuzo hiyo.

Mafanikio hayo yanaakisi hatua zinazotekelezwa na Benki Kuu katika kuimarisha mazingira ya kisera na kiudhibiti, kukuza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za fedha, kupunguza pengo la kijinsia na kuhakikisha huduma rasmi za fedha zinawafikia na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.

Pia yanaonesha maendeleo ya Tanzania katika kutekeleza ahadi za Azimio la Maya, linalohimiza taasisi wanachama wa AFI kuweka na kutekeleza malengo mahsusi na yanayopimika ya kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma jumuishi za fedha, pamoja na kupunguza pengo la kijinsia.

Jukwaa hilo liliandaliwa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI), inayojumuisha taasisi wanachama kutoka nchi 84, na lilihudhuriwa na zaidi ya washiriki 700 kutoka nchi 79.