Skip to content
Gavana Tutuba: Uchumi wa Tanzania waendelea kuimarika licha ya changamoto za dunia

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel M. Tutuba, amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuonesha uimara mwaka 2025 kwa kurekodi ukuaji wa asilimia 5.9, huku ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2026 licha ya changamoto zinazoendelea katika uchumi wa dunia.

Akizungumza katika Mkutano wa 29 wa Kamati ya Masuala ya Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (29th Monetary Affairs Committee – MAC), uliofanyika Julai 24, 2026 mjini Kampala, Uganda, Bw. Tutuba alisema matokeo hayo yanaonesha uwezo wa uchumi wa Tanzania kustahimili misukosuko ya kimataifa, ingawa bado kuna nafasi ya kuongeza kasi ya ukuaji ili kufikia wastani wa kabla ya janga la UVIKO-19 na lengo la ukuaji wa asilimia 7 lililowekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema mfumuko wa bei umeendelea kubaki ndani ya lengo la taifa la asilimia 3 hadi 5 na pia ndani ya vigezo vya muafaka wa EAC, licha ya kuongezeka kwa shinikizo lililosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta kufuatia mvutano wa kisiasa katika Mashariki ya Kati. Kutokana na hali hiyo, mfumuko wa bei uliongezeka hadi asilimia 4.2 mwezi Mei 2026 kabla ya kushuka kidogo hadi asilimia 4.0 mwezi Juni 2026.

Bw. Tutuba alisema ili kudhibiti athari za ongezeko la bei za mafuta katika uchumi wa ndani, Benki Kuu ya Tanzania iliongeza Kiwango Kikuu cha Riba (Central Bank Rate - CBR) kutoka asilimia 5.75 hadi asilimia 6.25.

Akizungumzia sekta ya nje, Gavana alisema nakisi ya urari wa akaunti ya sasa ilishuka hadi asilimia 2.2 ya Pato la Taifa mwaka 2025, kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka mitano. Hata hivyo, alisema misukosuko ya hivi karibuni katika uchumi wa dunia ilisababisha nakisi hiyo kuongezeka kidogo hadi asilimia 2.4 ya Pato la Taifa katika mwaka ulioishia Juni 2026.

Alisema Benki Kuu inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi pamoja na kuhimiza uzalishaji wa bidhaa zinazoweza kuchukua nafasi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Aidha, alisema akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuimarika kupitia mpango wa ununuzi wa dhahabu, ambapo akiba ya fedha za kigeni sasa imefikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 6, bila kujumuisha dhahabu ambayo bado haijageuzwa kuwa akiba ya fedha

 Aliongeza kuwa kiwango hicho kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.5, hivyo kukidhi kigezo cha EAC. Akijumuisha dhahabu ambayo bado haijageuzwa kuwa akiba ya fedha, akiba ya kimataifa ya Tanzania imefikia takribani dola za Marekani bilioni 8.7.

Kwa upande wa sera za fedha za Serikali, Bw. Tutuba alisema nakisi ya bajeti inakadiriwa kupungua hadi asilimia 3.1 ya Pato la Taifa katika mwaka wa fedha 2025/26 kutokana na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani na usimamizi madhubuti wa matumizi ya Serikali. Aidha, deni la umma linaendelea kuwa himilivu, likiwa katika asilimia 39.6 ya Pato la Taifa kwa thamani ya sasa, chini ya kiwango cha juu cha asilimia 50 kilichowekwa na EAC.

Gavana huyo pia alisema sekta ya fedha nchini inaendelea kuwa imara, salama na yenye uwezo wa kukabiliana na mishtuko ya kiuchumi. Alibainisha kuwa sekta ya benki imeendelea kupata faida na kuwa na mtaji wa kutosha kukabiliana na changamoto za muda mfupi, huku kiwango cha mikopo chechefu kikishuka hadi asilimia 2.9 kutoka kiwango cha juu cha asilimia 12.5 kilichorekodiwa mwaka 2017.

Alisema Benki Kuu itaendelea kutekeleza mageuzi yanayolenga kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha, kuboresha usimamizi wa taasisi za fedha na kulinda utulivu wa mfumo wa fedha nchini.

Akihitimisha hotuba yake, Bw. Tutuba alizitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kuwa makini kutokana na kuongezeka kwa hatari zinazoikabili dunia na kuelekeza mijadala katika kutafuta suluhisho zinazotekelezeka ili kuharakisha azma ya kuanzishwa kwa Umoja Kamili wa Fedha wa Afrika Mashariki.

Alisisitiza kuwa Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi nyingine za kikanda katika kuendeleza ajenda ya ushirikiano wa kikanda na kufanikisha malengo ya pamoja ya maendeleo ya uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.