Skip to content
Uthabiti wa Sekta ya Fedha
Utangulizi na Muhtasari

Uthabiti wa sekta ya fedha ni hali ambayo mfumo wa kifedha unaojumuisha taasisi za kifedha, masoko ya kifedha na miundombinu ya masoko ya kifedha una uwezo wa kuhimili mishtuko na mkusanyiko wa kutokuwiana kwa kifedha, huku ukiendelea kutoa huduma muhimu za kifedha kwa kaya, biashara na uchumi kwa ujumla.

Mfumo wa kifedha ulio imara na unaofanya kazi kwa ufanisi huchangia ukuaji endelevu wa uchumi kwa kuhakikisha kuwa upatanishi wa kifedha unafanyika kwa ufanisi na bila ya usumbufu mkubwa. Mfumo huo huwezesha kaya na biashara kuweka akiba, kukopa, kuwekeza, kujikinga dhidi ya hatari, kufanya malipo, kusimamia hatari na kupanga kwa ajili ya siku zijazo kwa kujiamini.

Utulivu wa kifedha si tu kutokuwepo kwa hali ya kuyumba kwa mfumo wa kifedha. Unahitaji uwepo wa mfumo wa kifedha ulio imara, wenye ustahimilivu na wenye uwezo wa kufyonza mishtuko hasi huku ukiendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi, hata wakati wa vipindi vya msongo wa kifedha.

Mifumo ya kifedha imeunganishwa kwa kiwango kikubwa, na kushindwa au matatizo yanayoikumba taasisi ya kifedha, soko la kifedha au mfumo wa malipo yanaweza kusambaa kwa haraka katika maeneo mengine ya mfumo wa kifedha. Kudumisha utulivu wa kifedha ni moja ya majukumu muhimu ya Benki Kuu na mamlaka za usimamizi wa sekta ya fedha. Hili linahusisha utambuzi, tathmini na ufuatiliaji endelevu wa udhaifu na hatari za kimfumo ndani ya mfumo wa kifedha, pamoja na utekelezaji wa hatua stahiki za kisera ili kupunguza hatari hizo na kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya fedha.


Dhamana ya uthibiti wa sekta ya fedha

Lengo kuu la Benki Kuu ya Tanzania, kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, ni kuandaa, kubainisha na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudumisha utulivu wa bei za ndani ili kuwezesha ukuaji wenye uwiano na endelevu wa uchumi wa taifa.

Katika kutekeleza jukumu hili, Benki pia ina wajibu muhimu wa kudumisha na kuendeleza utulivu wa kifedha kwa kulinda uimara na ustahimilivu wa mfumo wa kifedha wa nchi. Ili kutekeleza wajibu huu kwa ufanisi, Benki hufuatilia kwa karibu maendeleo ya uchumi mpana na mwenendo wa viashiria vya tahadhari za kiusalama za mfumo mzima wa kifedha (macroprudential conditions) katika sekta ya fedha.

Kupitia ufuatiliaji na uchambuzi wa kina unaofanyika kwa wakati, Benki hutambua, kutathmini na kupunguza hatari za kimfumo, na hivyo kuzuia kujengeka kwa udhaifu unaoweza kuathiri utendaji wa mfumo wa kifedha na kuwa na athari hasi kwa uchumi kwa ujumla.


Malengo na Majukumu

Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu muhimu katika kudumisha uthabiti na ustahimilivu wa mfumo wa kifedha nchini. Ili kutekeleza jukumu hili, Benki Kuu kupitia Idara yake ya Uthabiti wa sekta ya fedha, hufanya ufuatiliaji wa tahadhari wa hali ya kifedha kwa kiwango cha taasisi moja moja za fedha (microprudential surveillance) na kwa mfumo mzima wa kifedha (macroprudential surveillance), na hutekeleza majukumu yafuatayo:

  • Kufanya ufuatiliaji wa kina wa uthabiti wa mfumo mzima wa kifedha (macro-prudential surveillance) ili kubaini vihatarishi vinavyoweza kuathiri uthabiti wa sekta ya fedha vinavyotokana na mazingira ya kifedha ya kimataifa, kikanda na kitaifa.
  • Kufuatilia na kutathmini utendaji na udhaifu wa sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya mashirika yasiyo ya kifedha, kaya, sekta ya majengo na nyumba, benki, bima, masoko ya mitaji, mifuko ya hifadhi ya jamii, taasisi za fedha ndogo, vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) pamoja na miundombinu ya mfumo wa fedha.
  • Kuratibu maandalizi, usimamizi na utatuzi wa migogoro ya kifedha ili kuhakikisha mfumo wa fedha una uwezo wa kukabiliana na misukosuko na kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi.
  • Kutathmini ustahimilivu na uthabiti wa mfumo wa fedha inayoweza kujitokeza kutokana na mazingira ya ndani na nje ya nchi. Kuandaa na kupendekeza hatua za tahadhari za kupunguza hatari za kimfumo zinazoweza kuathiri uthabiti wa mfumo wa fedha.
  • Kutathmini hali ya uthabiti wa mfumo wa fedha na kuandaa Ripoti za Uthabiti wa Sekta ya Fedha pamoja na machapisho mengine kwa ajili ya wadau na umma.
  • Kuratibu ulinganifu wa mifumo ya uthabiti wa sekta ya fedha kwa kushirikiana na wasimamizi wengine wa sekta ya fedha nchini kupitia Jukwaa la Uthabiti wa Sekta ya Fedha Tanzania (Tanzania Financial Stability Forum - TFSF), pamoja na kushiriki katika mipango ya kikanda na kimataifa inayolenga kuimarisha na kuoanisha mifumo na mbinu za kudumisha uthabiti wa sekta ya fedha.

Udhibiti wa tahadhari katika ngazi ya mfumo mzima wa kifedha

Benki Kuu ya Tanzania hufuatilia na kutathmini utendaji, ustahimilivu na udhaifu wa sekta ya fedha nchini kwa lengo la kuendeleza utulivu wa kifedha. Katika kutekeleza jukumu hili, Benki ina nafasi muhimu katika kutathmini maendeleo mbalimbali na kubaini hatari zinazoweza kujitokeza ambazo zinaweza kuhatarisha utulivu wa mfumo wa kifedha.

Kama sehemu ya mfumo wake wa ufuatiliaji wa tahadhari za kiusalama za mfumo wa kifedha, Benki hufanya tathmini za mara kwa mara katika maeneo muhimu, ikiwemo hali ya soko la mikopo, taasisi za kifedha na zisizo za kifedha, mwenendo wa sekta ya kaya, maendeleo katika miundombinu ya mfumo wa kifedha pamoja na mwenendo wa soko la mali zisizohamishika.

Aidha, Benki hufanya majaribio ya msongo (stress tests) katika sekta ya benki kwa kuandaa na kuendesha mazingira ya kubuni yanayowakilisha mtikisiko mkubwa lakini unaowezekana kutokea katika uchumi, kwa lengo la kubaini udhaifu uliopo na kutathmini uwezo wa sekta hiyo kuhimili mishtuko inayoweza kujitokeza. Vilevile, Benki huchunguza kiwango cha muunganiko ndani ya mfumo wa kifedha ili kubaini njia zinazoweza kusababisha usambazaji wa hatari na maambukizi ya migogoro ya kifedha, pamoja na kuandaa viashiria vya uimara wa kifedha kwa ajili ya kufuatilia afya na utulivu wa sekta ya fedha kwa ujumla.


Ufuatiliaji na Upunguzaji wa Hatari katika Mfumo wa Fedha

Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu muhimu katika kulinda mfumo wa kifedha wa nchi dhidi ya misukosuko inayoweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi. Sehemu muhimu ya jukumu hili ni utambuzi, tathmini, ufuatiliaji, usimamizi na upunguzaji wa hatari za kimfumo zinazoweza kuhatarisha utulivu wa sekta nzima ya fedha.

Benki hufuatilia kwa karibu udhaifu unaojitokeza na kutathmini vyanzo vinavyoweza kusababisha hatari za kimfumo kutokana na maendeleo ya ndani ya nchi, kikanda na kimataifa. Kwa kuzingatia tathmini hizo, Benki huandaa na kutekeleza hatua stahiki za kisera pamoja na mikakati mingine ya kupunguza hatari kwa lengo la kudhibiti na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika mfumo wa kifedha. Aidha, Benki huendesha mazoezi ya kuigiza hali za migogoro ya kifedha (crisis simulation exercises) ili kupima ufanisi wa mifumo ya utayari na mwitikio katika kukabiliana na migogoro ya kifedha, kubaini mapungufu yanayoweza kujitokeza, na kuimarisha uratibu miongoni mwa wadau mbalimbali katika usimamizi wa migogoro ya kifedha.

Benki hutathmini kiwango cha uzingatiaji wa miongozo na mifumo mbalimbali inayohusu utulivu wa kifedha na usimamizi wa migogoro ya kifedha ili kuhakikisha kuwa taasisi za kifedha na wadau wengine husika wamejipanga ipasavyo kukabiliana na vipindi vya msongo wa kifedha.


Usimamizi wa Utatuzi wa Migogoro katika Mfumo wa Fedha

Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu la msingi katika kuhakikisha kuwa mfumo wa kifedha wa nchi unabaki kuwa imara na wenye ustahimilivu hata wakati wa vipindi vya msongo wa kifedha. Kama sehemu ya dhamana yake ya kudumisha utulivu wa kifedha, Benki imepewa jukumu muhimu la usimamizi na utatuzi wa migogoro ya kifedha, linalolenga kupunguza athari za matatizo ya kifedha kwa uchumi kwa ujumla na kudumisha imani ya umma katika mfumo wa kifedha.

Usimamizi madhubuti wa migogoro ya kifedha unahusisha mchanganyiko wa utambuzi wa mapema wa viashiria vya hatari, mifumo ya uratibu wa hatua za kukabiliana na migogoro pamoja na mifumo ya wazi ya utatuzi wa migogoro inayowezesha Benki kuchukua hatua kwa haraka na kwa ufanisi pindi kunapotokea hali ya kuyumba kwa sekta ya fedha.

Aidha, Benki hufanya tathmini ya uwezo wa kutatulika kwa taasisi za benki na taasisi nyingine za kifedha (resolvability assessment). Vilevile, kama sehemu ya zana zake za usimamizi wa migogoro ya kifedha, Benki Kuu ya Tanzania hutoa na kufuatilia kwa karibu Mfumo wa Msaada wa Dharura wa Ukwasi (Emergency Liquidity Assistance - ELA). Mfumo huu umeundwa kutoa msaada wa muda wa ukwasi kwa taasisi za kifedha zenye uwezo wa kuendelea kufanya kazi (solvent institutions) zinazokabiliwa na changamoto za muda mfupi za ukwasi, lakini ambazo misingi yake ya kifedha bado ni imara. Hali hii husaidia kuimarisha imani katika mfumo wa benki na kuendeleza utendaji wenye utaratibu wa masoko ya kifedha wakati wa vipindi vya msongo wa kifedha.


Jukwaa la Uthabiti wa Kifedha Tanzania

Katika kuimarisha uthabiti wa kifedha na ustahimilivu wa mfumo wa kifedha wa nchi, Benki Kuu ya Tanzania huratibu ushirikiano baina ya wadhibiti wa sekta ya fedha na taasisi nyingine muhimu zinazounda mtandao wa usalama wa kifedha. Ushirikiano huu unalenga kuhakikisha utambuzi wa mapema, pamoja na hatua za haraka na madhubuti dhidi ya maendeleo au matukio yanayoweza kutishia uthabiti wa mfumo wa kifedha.

Ili kuwezesha uratibu huu, Benki Kuu ya Tanzania ilianzisha na inaongoza Jukwaa la Uthabiti wa Kifedha Tanzania (Tanzania Financial Stability Forum) ambalo ni chombo rasmi cha mawasiliano, kubadilishana taarifa na kufanya maamuzi ya pamoja kati ya wadau wakuu wanaohusika na kulinda uthabiti wa mfumo wa kifedha nchini.

Wajumbe wa Jukwaa la Uthabiti wa Kifedha Tanzania ni:

  • Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
  • Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (MOF - URT)
  • Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (PO-FP RGoZ)
  • Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (PO–RALG)
  • Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Mahusiano (PMO-LER)
  • Ofisi ya Makamu wa Rais – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (VPO–URT)
  • Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA)
  • Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)
  • Tume ya Ushindani wa Haki (FCC)
  • Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
  • Bodi ya Bima ya Amana (DIB)
  • Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC)
  • Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT)
  • Kitengo cha Kijasusi cha Fedha (FIU)
  • Tume ya Mipango ya Taifa (NPC)

Ripoti na Machapisho

Benki Kuu ya Tanzania huchapisha ripoti na machapisho mbalimbali kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu maendeleo yanayojitokeza ndani ya mfumo wa kifedha wa nchi. Kupitia Idara ya Utulivu wa Kifedha, Benki huandaa na kuchapisha Ripoti ya Utulivu wa Kifedha ya Tanzania (Tanzania Financial Stability Report), ambayo hutoa taarifa kuhusu hali ya utulivu na ustahimilivu wa mfumo wa kifedha wa nchi kwa wadau mbalimbali, wakiwemo watunga sera, mamlaka za usimamizi wa sekta ya fedha, taasisi za kifedha, watafiti, wawekezaji na umma kwa ujumla.


Miongozo, Kanuni na Miundombinu ya Kisheria

Benki Kuu ya Tanzania imejikita katika kukuza mfumo wa kifedha ulio imara, jumuishi na endelevu. Kama sehemu ya jukumu lake kuu, Benki Kuu kupitia Idara ya Uthabiti wa Kifedha huandaa, hupitia upya, na kusambaza mara kwa mara miundombinu ya kimkakati, kanuni na miongozo inayosaidia kuimarisha uimara na uthabiti wa mfumo wa kifedha.